Hii ni Tahakiki ya msingi ya tamhiliya ya Orodha. Mwalimu au mwanafunzi wa kiswahili anaweza itumia kazi hii kujiandaa na mtihani wa kidato cha nne.
Inajumuisha sehemu ya maudhui tu. Sehemu ya pili ya uhakiki huu itajumuisha vipengele vya fani.
Karibu.
2. Utangulizi
Tamthiliya ya Orodha ni tamthiliya inayohusu suala zima la ugonjwa wa
UKIMWI na madhara yake katika jamii.
Mwandishi anaweka wazi kuhusu gonjwa hili. Mhusika mkuu Furaha
anaathirika na gonjwa hili na kufariki dunia.
Kimaudhui tamthiliya hii imesawiri maisha ya sasa ya jamii ya Watanzania
kwani ugonjwa huu bado ni tishio.
Kwa upande wa fani, mwandishi amewaumba vyema wahusika wake,
muundo wake ni unaomvutia msomaji kujua ni nini kingeendelea
mbeleni, ameteua lugha nzuri ya kisanaa. Haya yote yanajielekeza katika
uchambuzi tutaoenda kuufanya.
5. Maambukizi ya VVU na UKIMWI
UKIMWI ni kifupi cha Upungufu wa Kinga Mwilini. Hili ni gonjwa lilitingisha
jamii na kutangazwa kama janga la Taifa mwanzoni mwa miaka ya tisini
mpaka sasa.
Mwandishi anaiangalia jamii ya mtanzania na kuona kuwa kunauhitaji
mkubwa wa elimu juu ya ugonjwa huu.
Mwandishi ameonesha jinsi maambukizi ya UKIMWI yanavyoweza
kutokea katika jamii. Kupitia mhusika Furaha, Bwana Ecko, Padri James,
Kitunda na Salim mwandishi anaonesha jinsi gonjwa hili hatari
linavyoweza kuathiri jamii nzima kwa muda mfupi.
Dhamira hii inajitokeza katika jamii yetu.
6. Athari za makundirika
Vijana wa rika moja (marafiki) hushawishiana kufanya mambo pamoja.
Katika hali kama hiyo kuna uwezekano wakafundishana na kushawishiana
kufanya mambo mabaya.
Mwandishi anamtumia mhusika Mary anayemshawishi Furaha na
kumpeleka Baa kwa bwana Ecko. Huko anamuingiza katika ulevi na
kumshawishi kufanya ngono na watu wazima.
Tatizo la makundirika lipo kwenye jamii yetu. Vijana wengi hutumbukia
katika mambo mabaya kwa kufuata mkumbo wa marafiki.
7. Vishawishi
Hii ni hali ya kumfanya mtu kutenda jambo fulani.
Mwandishi ameonesha udhaifu wa binadamu katika ushawishi.
Anamtumia mhusika Padri James anayeshawishika kwa Furaha na kujikuta
akiingia katika dhambi ya ngono.
Pia mhusika Mary anamshawishi Furaha kumkubali Bwana Ecko na
kumuahidi kuwa atapata vitu vizuri.
Mwisho mhusika Kitunda anamshawishi Furaha kuvuta bangi na
kumshawishi wafanye ngono.
8. Hofu
Hofu ni hali ya kuwa na woga. Wahusika wanaonekana wakisongwa na
hofu juu ya orodha inayokwenda kusomwa.
Wanakijiji wote walikuwa na hofu kwa kuwa hawakuwa na taarifa za
kutosha juu ya ugonjwa wa UKIMWI. Mwandishi anaonesha jinsi hofu
inavyoweza kuathiri maisha ya mwanadamu.
Anaonesha jinsi Bwana Ecko, Juma, Padri James na Kitunda wanavyopata
shida kutafuta orodha.
Mwisho wa yote orodha hiyo haikuwa kama walivyofikiri wao.
9. Mmomonyoko wa Maadili
Maadili ni jumla ya taratibu jamii ilizojiweke ili watu wake wawe na
mwenendo mwema. Mwandishi anaiakosoa jamii kwa kuionesha jinsi
ilivyokengeuka kutoka katika maadili iliyojiwekea.
Anamtumia mhusika Furaha ambaye hukutoroka nyumbani na kwenda
kwenye sehemu za starehe. Kwa desturi za jmii yetu msichana wa rika la
Furaha haruhusiwi kwenda sehemu hizo. Pia, Furaha anajihusisha na vitendo
vya kihuni na kuidharirisha familia yake.
Vitendo vingine vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili ni pale;
Bwana Ecko na Juma ni wakubwa kiumri lakini wanajihusisha kimapenzi na
wasichana wadogo (Furaha na Mary).
Padri James anaitumia nafasi yake kama kiongozi wa dini kufanya ngono na
Furaha.
Furaha anapokutana na Salimu nyumba ya nyumba yao.
Matukio yote haya yaashiria kumomonyoka kwa maadili ya jamii.
10. Mapenzi ya kweli
Mapenzi ya kweli yamejidhihirisha kupitia mhusika Furaha kwa jamii yake.
Upendo huo umedhihirika pale alipoamua kuandikia jamii yake barua
yenye orodha ya mambo ya msingi ambayo yangeisaidia jamii kujiepusha
na maambukizi ya UKIMWI.
Mama Furaha anaonesha kuwa na upendo wa dhati na binti yake.
Alimuangalia kwa ukaribu na kumtunza hata pale alipogundua kuwa
alikuwa ameathirika na VVU. Alimpa tumaini mpaka siku yake ya mwisho.
Mama furaha alionesha kuwa na upendo wa kweli na jamii yake.
Furaha alionesha kuwa na upendo wa ukweli na jamii yake.
11. Umbeya na masengenyo
Umbeya ni tabia ya kutoa habari bila ya kutumwa.
Mwandishi anaonesha tabia hiyo kupitia wanakijiji, wanakijiji wanatabia za
umbea na masengenyo sana. Mfano katika Uk 18 Mwanakijiji wa 3
anampasha habari Mama Furaha juu ya umbea uliozagaa kijijini kwao
kuhusu Furaha.
Pia, baada ya kuugua kwa Furaha habari zilizagaa kijijini kuwa ameandaa
orodha itakayosomwa kwa sauti siku ya mazishi yake.
Tabia za namna hii zipo miongoni mwa wanajamii wenzetu.
12. Kukata Tamaa
Kukata tamaa ni kitendo cha kuacha kuwa na shauku ya kufanya jambo
Fulani zaidi. Kitendo cha Furaha kuandika orodha baada ya kujua kuwa
anaugua UKIMWI kinaonesha kuwa alikuwa amekata tamaa.
Hakuona tumaini la maisha tena baada ya kugunduliwa ameathirika na
virusi vya UKIMWI.
Watu wengi kwenye jamii yetu hujikuta wakikata tamaa
wanapogundulika kuwa wameathirika na UKIMWI.
13. Tamaa
Kila binadamu huwa na matarajio ya kupata kitu fulani.
Furaha alijiingiza katika vitendo vya ngono na bwana Ecko kwa kutamani
pesa zake.
Pia, Furaha alijikuta yumo kwenye mtego wa Kitunda kwa kutamani vitu
alivyonavyo; kama sterio na vinginevyo.
Mwandishi anaikemea tabia hii na kubainisha kuwa ni moja ya chanzo
cha maambukizi kwa vijana.
14. Umalaya (Ukahaba)
Hii ni tabia ya baadhi ya watu wanaoshiriki vitendo vya ngono na watu
wengi kwa dhumuni la kulipwa pesa au starehe.
Mhusika mkuu, Furaha anajihusisha na vitendo vya ngono na watu wengi
kijijini kwao.
Pia, Bwana Ecko anajihusisha na vitendo vya ngono na wasichana wengi
hapo kwa kijijini.
Wapo vijana wanaojihusisha na tabia za kikahaba katika jamii zetu
15. Unyanyapaa
Kunyanyapaa ni kumuepuka mtu na kumuona kinyaa.
Wanakijiji wanogopa kukutana na mtu aliyeambukizwa maradhi ya
UKIMWI kwa kuwa wanaamini wataambukizwa.
Salim anapomtembelea Furaha anaogopa kukaa naye karibu au
kumshika mkono kwa kuwa anahofia kuwa ataambukizwa VVU.
Hivyo mwandishi ameona tatizo hili la unyanyapaa katika jamii yetu na
kuliweka bayana.
16. Imani Potofu
Hizi ni imani zisizo za ukweli. Jamii mara nyingine hujijengea imani juu ya
jambo Fulani bila kuwa na uhakika au uthibitisho juu yake.
Mhusika mwanakijiji wa kwanza anapendekeza kuwa Furaha alipata
ugonjwa kwa kurogwa.
Bwana Juma anaamini ukifanya mapenzi na msichana bikira ni dawa ya
UKIMWI.
Hii inaonesha kuwa watu wengi hawana elimu ya kutosha juu ya ugonjwa
wa UKIMWI.
17. Kukosekana kwa elimu Juu ya
ugonjwa wa UKIMWI
Gonjwa la UKIMWI ni gonjwa jipya kwenye jamii ya waafrika. Hivyo watu
wengi hawajui mambo mengi kuhusu ugonjwa huu.
Mwandishi anaonesha kuwa wanakijiji hawajui masuala mengi
yanayohusiana na ugonjwa wa UKIMWI; ikiwemo namna unavyoenezwa,
tiba na namna ya kujikinga.
Wanatoa mawazo mengi ambayo si ya kweli juu ya ugonjwa huu hatari.
Tatizo hili lipo zaidi katika maeneo ya vijijini nchini Tanzania.
19. Migogoro
Mgogoro kati ya Furaha na Dada Mdogo
Mgogoro huu umejitokeza pale Furaha alipokuwa anatoroka usiku kwenda
baa.
Mgogoro kati ya Baba Furaha na furaha
Mgogoro huu umetokea baada ya baba kugundua kuwa furaha huwa
anatoroka usiku.
Mgogoro kati ya Furaha na Salim
Mgogoro huu unajitokeza pale Salimu anapoenda kuulizia orodha kwa
Furaha.
Mgogoro kati ya bwana Juma na Mary
Mgogoro kati ya Salim na Mama Furaha
Baada ya Salim kuchana barua iliyokuwa imeshikwa na mama Furaha.
20. Ujumbe
Tamaa mbele mauti nyuma
UKIMWI huathiri watu wa rika zote
Mapenzi ya utotoni si mazuri katika jamii
Tunatakiwa tuwatii wazazi na kufanya kazi kwa bidi
Marafiki wabaya hutupeleka katika njia isiyofaa
Matumizi ya kondomu hupunguza maambukizi ya UKIMWI
Dhana potofu hupelekea unyanyapaa
21. Falsafa
Mwandishi anaamini kuwa Binadamu ni kiumbe dhaifu sana kisichoweza
kupingana na vishawishi. Anamtumia mhusika furaha na Padre James
ambao wanashindwa kupambana na tamaa za miili yao na kujikuta
wakiingia katika vitendo vya ngono. Matokeo yake ni kuongezeka kwa
maambukizi ya UKIMWI.
Pia mwandishi anaamini kuwa watu wakipata elimu juu ya ugonjwa wa
UKIMWI tunaweza kupunguza mambukizi mapya. Anatoa mapendekezo
yatakayoiokoa jamii yake kwa kutumia orodha ya mambo ya msingi ya
kuzingatiwa.
22. Mtazamo
Mwandishi anamtazamo yakinifu. Anaiangalia jamii yake katika mtazamo
dhahiri wenye uthibitisho.
Anabainisha changamoto zinazoikumba jamii yake na kuonesha
suluhisho la matatizo hayo.
Mfano anaonesha tatizo la jamii kukosa elimu ya ugonjwa wa UKIMWI na
kutoa namna ya kuliepuka janga hilo.
Mwandishi anamtazama Padri James kwa jicho la kibinadamu. Anamuona
kama binadamu mwingine na kwamba anaweza kuathiriwa na tamaa za
kibinadamu.
23. Swali
“Mwandishi ni mwanga wa jamii,
unaomulika katika kiza kinene cha ouvu.”
Jadili kauli hii kwa kutumia tamthiliya mbili
ulizosoma darasani.